……Kwa vipindi mbalimbali ndani ya muda usiozidi miezi mitatu, wadau wa Kiswahili walioteuliwa na jopo la wataalamu wa Kiswahili watazuru na kukaa kwenye asasi mbalimbali katika JAM ambazo zinatumia na kuendeleza Kiswahili. Lengo la mpango mzima ni kutoa fursa kwa walioteuliwa na wenyeji wao, pamoja na wadau wengine wa Kiswahili kushirikiana na kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo na matumizi ya Kiswahili. Ili kufanikisha hilo, kila mdau alipendekeza shughuli ya kufanya na ambayo iliidhinishwa na kufadhiliwa na KAKAMA.

Inategemewa kwamba baada ya muda waiotengewa, kila mmoja wa wadau hao ataandika ripoti kuhusu tajriba yake pamoja na kutoa mapendekezo ya kuufanya bora zaidi mpango huo. Ripoti hiyo pia itaonyesha namna ambavyo KAKAMA kupitia Mpnago wa ubadilishanaji wadau inavyoweza kuchangia kujenga utangamano miongoni mwa wananchi wa JAM.

Jumla ya maombi 126 (mia moja ishirini na sita) yalipokelewa: 123 (mia moja na ishirini na tatu) yalikuwa ya watu binafsi na 3 (matatu) kutoka kwa asasi. KAKAMA ilidhamini watu binafsi 23 (ishirini na tatu) na asasi 3 (tatu).

Hongereni Washindi!!!!!

Khadija Juma ABDALLA ni mdau wa Kiswahili kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Tanzania. Khadija ana shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na ni mwalimu wa Kiswahili katika shule ya Sekondari ya Vikokotoni. Khadija atakuwa Chuo Kikuu Cha Bishop Stuart, Mbarara, nchini Uganda ambako atasaidiana na wenzake kuutathmini mtaala wa Kiswahili. Aidha, Khadija atafanya uchunguzi wa muda mfupi wa mielekeo kuhusu Kiswahili kama lugha ya mawasiliano mapana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

B-P: khadijaabdallah234@gmail.com

Monday Geofrey Akol AMAZIMA ni mwalimu, mwanahabari, mwandishi na mkereketwa wa kukiendeeza Kiswahili nchini Uganda, Afrika Mashariki na barani Afrika. Kwa sasa Monday ni Mtayarishaji vipindi na mtangazaji wa Kiswahili katika Shirika la Utangazaji la Uganda la UBC na ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ndejje, Uganda. Katika Programu ya kubadilishana wadau, Monday yuko  shirika la habari la ITV, Dar es salaam, Tanzania.

B-P: mwalimakol@gmail.com

Caroline ASIIMWE ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Kwa muda wa miezi miwili, Caroline atajiunga na Chuo Kikuu cha Kibabii mjni Bungoma nchini Kenya ambako atashirikiana na wenyeji wake katika kuandika makala za pamoja za kitaaluma kuhusu maendeleo na matumizi ya Kiswahili, pamoja na kuona namna Idara ya Kiswahili inavyoongozwa katika mfumo mzima wa utawala wa Chuo Kikuu cha Kibabii.

B-P: ncasiimwe@gmail.com 

Chantal BIRARONDERWA ni mwalimu wa Kiswahili shule ya Sekondari ya COMIBU- BUYENZI ,mjini Bujumbura, Burundi. Chantal alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Burundi, Kitivo cha Lugha na Sanaa za Kiafrika. Akiwa MS TCDC, Arusha, Tanzania kwa mwezi mmoja, Chantal atahudhuria vipindi vya Kiswahili kwa wageni pamoja na kutangamana na walimu na wanafunzi wengi wa kigeni ili kujiimarisha kimawasiliano.

B-P: birarondegwachantal@gmail.com

Prosper BUKURU ni mwanahabari wa Kiswahili katika kituo cha Redio cha Eagle Sport FM. Kabla ya hapo, Prosper, ambaye ni mtangazaji maarufu wa michezo, alifanya kazi Star FM. Mbali na vipindi vya michezo, Prosper pia hushiriki vipindi vingine vya redio ambavyo hutumia Kiswahili. Akiwa UBC, Uganda, Prosper ataendeleza kipaji cha utangazaji kupitia Kiswahili.

B-P: prosperemileck@yahoo.com

Dkt. Mahmoud Yussuf HAJI ana  shahada ya Uzamifu katika Kiswahili na ni mwalimu wa shule ya Sekondari ya Tumekuja. Mahmoud atakuwa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, Kenya kwa mwezi mmoja atakakobadilishana mawazo na uzoefu na walimu na wanafunzi wa Kiswahili. Aidha, Mahmoud ataichunguza mitaala ya Programu za Kiswahili za Shahada ya BA na Shahada ya Elimu (BEd).

B-P: Mahmoudhaji89@gmail.com

Moh’d Idrisa HAJI ni Mwalimu wa Kiswahili shule ya Sekondari ya Mtule, Zanzibar, Tanzania. Moh’d ana shahada ya Uzamili katika Kiswahili. Kwa mwezi mmoja, Moh’d atakuwa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, Kenya ambako anatarajia kujifunza kuhusu maendeleo na matumizi ya Kiswahili katika mazingira rasmi ya Chuo na mazingira yasiyo rasmi nje ya Chuo kikuu.

B-P: mohamedidrisa@hotmail.com

ulfat

Ulfat Abdullaziz IBRAHIM ni mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sumait, Zanzibar na mwanafunzi wa Uzamifu katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Ulfat atakuwa Chuo Kikuu cha Moi, Bewa la Coast, mjini Mombasa ambako atajishughulisha na masuala ya maendeleo na matumizi ya Kiswahili. Mbali na kutangamana na walimu na wanafunzi wa Kiswahili, Ulfat pia atatumia muda wa mwezi alionao Mombasa kudadavua data za utafiti wa shahada yake ya uzamifu.

B-P: madamullu@gmail.com

Riziki JACOB ni mwanahabari wa Kiswahili kwenye kituo cha Radio Eagle kilichoko Makamba, Burundi. Riziki amejiunga na Shirika la Utangazaji la Uganda (Uganda Broadcasting Corporation – UBC) kwa muda wa mwezi mmoja kwa lengo la kushiriki katika shughuli za maandalizi ya habari za Kiswahili. Riziki anatarajia kunufaika kutokana na maarifa na stadi za kuandika, kuhariri na kutangaza habari za Kiswahili. Vilevile, anatarajia kujenga uhusiano baina ya vituo hivi vya habari.

B-P: jacobriziki@yahoo.com

Kibigo Mary LUKAMIKA ni mwalimu wa Kiswahili katika shule ya msingi ya Ebusakami, katika Kaunti ya Vihiga, nchini Kenya. Kibigo ana Shahada ya Uzamili katika Kiswahili na amekuwa akifundisha shule za msingi mbalimbali na kuwawekea wanafunzi msingi imara katika Kiswahili. Yeye husahihisha Kiswahili katika viwango mbalimbali vya utahini. Kutokana na ujuzi na tajriba yake, na wakati akipata nafasi, Kibigo husaidia kufunza Kiswahili katika vyuo vikuu kadhaa. Kwa mwezi mmoja, Kibigo atakuwa MS TCDC, Arusha ambako atatangamana na wenyeji wake na wanafunzi wa kutoka nje ya Afrika katika programu ya Kiswahili kwa wageni ili kujifunza utekelezaji wake na mchango wa kukisambaza Kiswahili duniani.

B-P: kibigomary@gmail.com

Mosol KANDAGOR ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika, Chuo Kikuu Moi, Kenya.  Dkt. Kandagor atakuwa katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda akishirikiana na wenzake katika kuutathmini Mtaala wa Kiswahili.  Aidha, Dkt. Kandagor atatumia kipindi hicho cha mwezi mmoja kuhariri na kuandaa kwa uchapishaji makala za CHAKAMA na CHAKITA.

B-P: mosolkandagor@gmail.com

Olivia KANWA ni mhadhiri katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Agustino Mtwara, Tanzania. Olivia ana ujuzi wa kufundisha Kiswahili kayika ngazi na viwango mbalimbali vya elimu. Mbali na kufndisha, Olivia anachunguza namna Kiswahili kinavyotagusana na kuchangia kuendeleza utamaduni wa jamii mbalimbali zikiwemo za Wamakonde, Wamwera na Wamakua wapatikanao Lindi na Mtwara. Wakati wa kipindi chake cha mwezi mmoja atakapokuwa Chuo Kikuu cha Bishop Stuart, Uganda, Olivia atashirikiana na wenyeji wake kuandaa mtaala wa Kiswahili, pamoja na kufanya utafiti kujua mwitikio wa wanafunzi kuhusu taaluma ya Kiswahili.

B-P: kanwaolivia@yahoo.com

Abraham Kubakurungi KYANGUNGU atakuwa Chuo Kikuu cha Moi mjini Eldoret nchini Kenya kwa muda wa mwezi mmoja. Yeye ni Mhadhiri na Mkuu wa Kitengo cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Bishop Stuart mjini Mbarara, Uganda. Abraham ana Shahada ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Kwa miaka 18 sasa, Abraham amehusika katika kuendeleza Kiswahili kupitia ufundishaji kwenye ngazi mbalimbali za elimu, uhariri, ukalimani, tafsiri, uhakiki, na uinjilisti. Wakati akiwa Chuo Kikuu cha Moi, Abraham ananuia kuijfunza namna ya kuisuka na kuiandaa mitaala ya Kiswahili kwa lengo la kupata maarifa atakayotumia akirudi chuoni kwake. Aidha, atashiriki shughuli nyingine za kuendeleza Kiswahili ikiwa ni pamoja na kutangamana na walimu na wahadhiri wenyeji wake.

B-P: kubakurungiabraham@gmail.com

Saade Said MBAROUK ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sumait, Zanzibar, Tanzania.  Mbarouk amehitimu ngazi ya Uzamili na kwa sasa anaendelea na shahada ya Uzamifu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Kwa muda wa mwezi mmoja, Mbarouk atakuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro mjini Kakamega, Kenya ambako atapata muda wa kuzichunguza kozi za Kiswahili zinazofundishwa pale. Mdau huyu pia atapata muda wa kuiendeleza kazi yake ya utafiti.

B-P: khasma10@yahoo.com 

Dkt. Arnold B. G. MSIGWA ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taasisi ya Taaluma za Kiswahili-TATAKI). Alihitimu shahada ya kwanza (Ualimu) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2008 na shahada ya Umahiri (Kiswahili) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2011. Alihitimu pia shahada ya Uzamifu (Kiswahili) mwaka 2016 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uwanja aliobobea ni Ujifunzaji wa Lugha ya Pili lakini anapendelea pia nyanja za Isimu Tumizi, Mofolojia na Leksikografia. Katika mpango huu wa ubadilishanaji wadau Arnold ataenda Chuo Kikuu cha Burundi kwenye Taasisi ya  Ecole Normale Superiore (ENS) ambako atasaidia kufundisha wanafunzi wa shahada ya Umahiri, kudurusu programu za Umahiri na kwa Shahada ya Awali.

B-P: agawasike@gmail.com

Nyakoda Joak MUNDIT ni mkereketwa wa Kiswahili na mwandishi chipukizi kutoka Juba, Sudan Kusini. Yeye huandika kusimulia hadithi fupi za vijana na wanawake wa Sudan Kusini. Nyakoda atakuwa Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) wakati wa kipindi chake cha kubadilishana wadau. Ananuia kujiimarisha kimawasiliano na kimaandishi ili aweze kupata maarifa zaidi ya kueleza nafasi ya vijana na wanawake wa Sudan Kusini katika utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

B-P: beckymundit40@gmail.com

Issaac MUMENA ni mwanahabari mashuhuri wa Kiswahili wa muda mrefu. Isaaca kwa sasa ni mwandishi  wa Kiswahi BBC Kampala, Uganda. Majukumu yake ni pamoja na kuandaa vipindi vya habari pamoja na kuhariri habari za Michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa vyombo vya redio na Televisheni vya BBC. Kwa mwezi mmoja, Isaac atakuwa Radio Free Africa, Mwanza, Tanzania ambako atabadilishana uzoefu na maarifa kwenye tasnia ya Kiswahili, Michezo na Maendeleo Afrika Mashariki.

B-P: ismumena@gmail.com

Boaz MUTUNGI ni mhadhiri wa Kiswahili katika Idara ya Lugha za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Kwa sasa, Boaz anafanya utafiti wa shahada ya Uzamifu katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ambako mada yake inahusu ‘Uchanganuzi tunduizi kilongo wa unyanyasaji wa kiusemi baina ya wanandoa katika tamthilia teule za Kiswahili.’ Hivyo basi, Boaz atakuwa MS TCDC Arusha ili kuzamia utafiti wake kwa kujadiliana na walimu na wanafunzi wa kozi zinazohusiana na masuala ya lugha na jinsia, pamoja na kuwasilisha matokeo ya awali ya utafiti wake.

B-P:  mtungib@chuss.mak.ac.ug 

Anicet NDAYIKENGURUTSE alikuwa mkereketwa wa Kiswahili kutoka nchini Burundi aliyetuma maombi na kuteuliwa kushiriki Mpango wa kubadilishana wadau. Kwa bahati mbaya, Anicet alituacha na kutangulia mbele ya hukumu kabla ya kushiriki Mpango. KAKAMA inasikitishwa na kifo cha ghafla cha Anicet. Daima tutauenzi mchango wake wa kukiendeleza Kiswahili Burundi na Afrika Mashariki kwa jumla.

Sarah Ndanu Mwangangi NGESU ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha South Eastern Kenya na mwanafunzi wa Uzamifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Sarah ni mtafsiri wa Kiswahili, Kiingereza na Kikamba na ana shahada mbili za uzamili katika Kiswahili na tafsiri kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi. Kwa sasa, Sarah ameandika makala za ktaaluma kuhusu tafsiri ya Kiswahili na kwa sasa anabobea katika mikakati ya tafsiri katika ufundishaji wa Kiswahili. Kwa mwezi mmoja, Sarah atakuwa katika , Arusha, Tanzania ambako atatangamana na walimu wa Kiswahili kwa wageni na wanafunzi kutoka nje ya Afrika ambao wapo pale kwa ajili ya kujifunza Kiswahili. Sarah anatarajia kujifunza namna tafsiri ina mchango katika kusambaza na kueneza Kiswahili duniani.

B-P: sarahngesu@gmail.com

Edith NIBAKWE ni mwandishi wa habari wa  Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International/RFI, Rwanda. Yeye pia ni mhariri wa Habari na vipindi kwenye kituo cha Kikristo cha Redio na Televisheni cha Authentic mjini Kigali. Edith amepata tajriba ya kutumia Kiswahili wakati akifanya kazi na Radio RPA ya Burundi, Radio Maendeleo ya mjini Bukavu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Radio Izuba na Radio Isango Star za Kigali. Mdau huyu atakuwa kituo cha habari cha ITV mjini Dar-es-Salaam, Tanzania kwa muda wa miezi miwili ili kujiimarisha katika maandalizi na uwasilishaji wa habari na vipindi vya Kiswahili.

B-P: nibakwe@gmail.com

Hussein NTAHOMBAYE atajiunga na Shirika la Radio Free Africa (RFA) nchini Dodoma, Tanzania kwa kipindi cha mwezi mmoja. Yeye ni mwanahabari wa Kiswahili wa shirika la kibinafsi la Redio na TV Rema, nchini Burundi. Kabla ya hapo, Hussein alifanya kazi na Redio ya Taïfa ya Burundi, RTNB na redio ya umma, RPA. Hussein amekuwa mjumbe wa Baraza la Utangazaji nchini Burundi na ametumia Kiswahili kutangaza amani na utangamano nchini Burundi. Akiwa RFA, Hussein atajiendeleza katika matumizi ya Kiswahili kujenga utangamano kitaifa na kikanda.

B-P: ntahombayehussein@gmail.com

Dkt Patrice NTAWIGIRA ni Mhadhiri wa Masomo ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Rwanda. Patrice ana shahada za MA na PhD kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nchini Tanzania. Mbali na kufundisha Kiswahili chuoni, anashirikiana sana na wakuza-mitaala ya Kiswahili nchini Rwanda. Patrice atakuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa mpango huu wa ubadilishanaji wa wadau wa Kiswahili.

B-P: ntapa2000@gmail.com

Dkt. Robert W. Oduori ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Kiswahili na Lugha Nyingine za Kiafrika ya Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, Kenya. Oduori amebobea katika isimu-Jamii na Fasihi ya Kiswahili na atakuwa Chuo Kikuu cha Burundi kwa miezi mitatu ambapo atafundisha Kiswahili na kusaidiana na wenyeji wake katika kuitathmini Mitaala ya Kiswahili. Aidha, Oduori atasaidia kuwaelekeza wanafunzi wa Uzamili kunoa mada zao na kuziwasilisha

B-P ocholit@yahoo.com